Header Ads

Breaking News
recent

MAFANIKIO YA BIASHARA, WAZO LA BIASHARA

Kuna watu ambao wamekuwa wanaanzisha biashara ambazo ukiziangalia tangu mwanzo unajua hazitaweza kudumu kwa muda mrefu, au zitawaletea changamoto nyingi katika kuziendesha biashara hizo. Hii ni kwa sababu mawazo yao ya biashara yanakuwa siyo bora na ya kipekee, yanakuwa hayaendani na biashara inayoweza kuwa na mafanikio makubwa na hivyo kushindwa kuwafikisha kwenye mafanikio ya kibiashara.
Iwe ndiyo unataka kuanza biashara au umeshaanza biashara, unahitaji kuwa na wazo zuri na la kipekee la biashara yako, na kuendelea kuboresha biashara yako kadiri siku zinavyokwenda.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri ili kupata wazo bora la biashara wanahitaji kuwa wabunifu wakubwa, au wawalipe watu ndiyo wawapatie wazo bora la biashara. Japo hayo yote yanawezekana, lakini pia hapo ulipo unaweza kuja na wazo zuri na bora sana la kibiashara, kama ukiwa mtu wa kufikiri sawasawa kulingana na mazingira uliyopo.
Zifuatazo ni njia tano za kujua kama wazo lako la biashara ni bora na litakuletea mafanikio.
  1. Hakuna mwingine anayefanya biashara kama hiyo.
Kama hakuna mtu mwingine anayefanya biashara kama unayofanya wewe au unayotaka kufanya wewe, basi wazo lako la biashara ni la kipekee. Hapa unakuwa umeangalia eneo ambalo bado halijaguswa na wengine, na iwapo utajipanga vizuri basi utaweza kutengeneza biashara ya kipekee.
Lakini pia ni muhimu kujua biashara unayofanya na kwa eneo unalotaka kuanzisha, siyo tu kwa sababu watu hawafanyi ndiyo ufurahie, huenda hakuna wateja kwa eneo hilo, soma namba 3 kujua zaidi.
  1. Wapo wanaofanya, lakini siyo kama unavyofanya wewe.
Kwa ulimwengu wa sasa, ni vigumu sana kuja na biashara yako pekee, yaani ukawa ni wewe tu unafanya biashara hiyo. Sasa hivi karibu kila biashara imeshafanywa kila mahali, hivyo usiache kufanya biashara kwa sababu kila mtu anafanya. Badala yake angalia wengine ni kipi ambacho hawafanyi, na anza kukifanya hicho.
Hapa unaangalia kwenye biashara hiyo mnayofanya, ni maeneo gani ambayo watu wengine wana madhaifu na wewe unajipanga kuyatumia madhaifu hao kujenga biashara yako. angalia ni vitu gani ambavyo wateja wanavikosa kisha wapatie wateja vitu hivyo. Leta utofauti kwenye biashara ambayo kila mtu anaifanya na utaweza kujijengea biashara ya kipekee.
  1. Inatatua tatizo.
Msingi mkuu wa biashara yoyote ni huu; kutatua tatizo. Hapa unatatua tatizo ambalo watu wanakuwa nalo, au unawapatia mahitaji yao. Kama unataka kujua iwapo wazo lako la biashara ni bora na la kipekee, jiulize ni matatizo yapi ya wateja wako ambao unayatatua kupitia biashara yako.
Ili kujua matatizo unayotatua, ni lazima uwajue wateja wa biashara yako ni watu gani, wanapatikana wapi na unawezaje kuwafikia. Unapotatua tatizo kubwa na linalowaathiri wengi, ndivyo unavyotengeneza biashara kubwa.
  1. Inadhaminika.
Kama ukitaka kujua wazo lako la biashara ni bora, ni kama linaweza kudhaminika. Kama unaweza kumweleza mtu kuhusu wazo hilo na namna ambavyo anaweza kulidhamini au kulipatia fedha na akashawishika kufanya hivyo, basi wazo hilo ni bora. Jambo muhimu kujua hapa ni namna gani ambavyo mtu anaweza kunufaika kupitia biashara hiyo.
  1. Ni rahisi kueleweka.
Watu wamekuwa wakitumia kauli hii ya utani lakini ina maana kubwa sana; kama huwezi kumweleza bibi au babu yako asiyejua kusoma wala kuandika ni biashara gani unafanya na unanufaikaje na akakuelewa, hujui biashara unayofanya. Ni utani lakini una ukweli, kama wazo lako la biashara halieleweki kwa urahisi, unakuwa kwenye wakati mgumu kuweza kuliuza kwa wengine. Hata kutangaza biashara yako kwa wateja wako itakuwa vigumu.
Hayo ndiyo mambo matano muhimu kuzingatia kwenye wazo lako la biashara ili uweze kujenga biashara bora na yenye mafanikio. Yafanyie kazi ili uweze kutengeneza biashara kubwa itakayokunufaisha wewe na wale wanaokuzunguka.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.